WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewataka Watanzania kujenga
utamaduni wa kuchangia elimu, kama wanavyofanya katika harusi. Kauli
hiyo aliitoa Dar es Salaam jana wakati wa Mahafali ya Darasa la Saba na
Shule ya Awali ya Shule ya Mwalimu Nyerere.
Alisema imekuwa jambo la kawaida kwa sasa, kukuta kundi la watu wamekaa kujadili michango ya harusi na kuacha elimu.
“Jamani
mimi nimetembea sijaona mambo yanavyofanyika hapa Tanzania, majirani
zetu tu hapo Kenya wanatushinda, Kenya hukuti watu wanachangisha harusi,
kule ukikuta watu wamekaa ujue wanajadili suala la elimu.
“Hapa
kwetu masuala haya ya harusi yanazidi kushamiri, zamani tulikuwa tunaona
wasichana ndiyo wanafanyiwa kitchen party, lakini eti sasa hivi wanaume
nao wanafanyia sijui begi party. Itafika mahali watu wataanzisha
kaptula party.
“Watanzania tumeacha kabisa kuchangia elimu,
tunaona harambee muhimu ni harusi, hebu tubadilike ndugu zangu, ukiona
jirani yako au ndugu yako anashindwa kusomesha mtoto msaidie,” alisema
Dk. Mwakyembe.
Aidha, alitoa wito kwa wanafunzi wa kike, kutokimbilia ndoa za utotoni na badala yake waweke juhudi katika masomo.
“Nawaasa
wanangu wote, lakini zaidi ninyi wa kike ogopeni ndoa za utotoni,
wekeni juhudi katika masomo mpate shahada nyingi zaidi, kwa kuwa sasa
hivi tuko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na ushindani wa ajira
utakuwa mkubwa,” alisema Dk. Mwakyembe.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Mwalimu Nyerere, Jenerali Ulimwengu,
alisema shule hiyo imeweza kukua kwa haraka toka wanafunzi 32
ilipoanzishwa hadi sasa ina zaidi ya wanafunzi 1,000, ambapo wanafunzi
127 wamehitimu darasa la saba kwa mwaka huu.
Wednesday, October 17, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment