Tuesday, October 30, 2012

Wassira aipinga Serikali yake

KATIKA kile kinachoonesha kuwapo msigano kwenye Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira, amepinga mfumo wa utungaji mitihani unaotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Mfumo huo mpya unaotumika sasa, unamtaka mtahiniwa kuchagua jibu sahihi na kuandika herufi kwenye namba ya swali katika masomo yote, jambo ambalo Waziri Wassira alidai halijawahi kutokea katika kipindi cha miaka yote hata wakati akisoma.
Wassira anakuwa waziri wa pili wa serikali ya Kikwete kupinga hadharani mfumo huo, akitanguliwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, ambaye alisema unadumaza elimu na kuongeza idadi ya wahitimu wasiojua kusoma na kuandika.
Wassira alisema hayo juzi katika mahafali ya kidato cha nne na sita ya Shule ya St. Anne Marie Academy, mara baada ya Mkurugenzi wa shule hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza, kulalamikia utaratibu huo.
Alisema hakubaliani na mitihani ya kuchagua na kwamba hoja hiyo ataifikisha katika mamlaka husika ili ifanyiwe kazi.
”Unajua ni jambo la kushangaza sana, mimi sidhani kama mwanafunzi atashindwa kubahatisha, lazima atabahatisha tu, ingekuwa vizuri mwanafunzi anafanya insha kama sisi zamani, hii inamjengea upeo mpana wa kuwa na uelewa zaidi,” alisema Wassira.
Wassira aliongeza kuwa wiki iliyopita serikali ilikutana mjini Dodoma kujadili vipaumbele mbalimbali vya kufanyia kazi katika miaka mitatu, ambapo pia lilizungumzwa suala zima la elimu na maboresho yake, kwamba anaamini mambo muhimu yatazingatiwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Wassira alilaumu wanafunzi kutofundishwa historia ya nchi yao huku akishangaa baadhi ya watu hata waliomaliza chuo kikuu kutojua vema historia, ikiwamo hata Uhuru na Muungano vilipatikana lini na kwa sababu gani.
Kauli hiyo hata hivyo ilitafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni kijembe kwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, ambaye aliwasilisha mada kwenye mkutano wa kimataifa na kudai kuwa Tanzania ni muungano wa visiwa vya Bahari ya Hindi vya Pemba, Tanganyika na Zimbabwe.
“Hili ni jambo la kushangaza kabisa mtu anashindwa kujua hata historia ya nchi yake ilikuwaje hadi tukaungana, uhuru lini na ndiyo maana utakuta wengine wanasema kuwa serikali tangu ipate uhuru haijafanya kitu chochote,” alisema Wassira.
Aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto muda wote ili kuwajenga katika maadili yaliyo mema na si kumwachia mwalimu pekee.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Johanssen Rwebugisa, alieleza mafanikio mbalimbali waliyoyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001, sambamba na changamoto zinazowakabili.
Alisema wamefanikiwa kuingia katika 10 bora ya shule jijini Dar es Salaam na kwamba ilianza na wanafunzi 45, lakini sasa zaidi ya wanafunzi 800 wanaendelea kujiunga kila mwaka.
Kuhusu changamoto, alisema ukosefu wa maji kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Taka Dar es Salaam (DAWASA), umekuwa kikwazo kwao na wananchi wote wa maeneo yanayoizunguka shule hiyo.
Naye Mkurugenzi wa shule hiyo, Rweikiza, aliitaka serikali kutilia maanani suala zima la mfumo wa mitihani ya kuchagua jibu sahihi pamoja na suala la lugha ya kufundishia kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.

CHANZO:TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment