Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa (kati) akitangaza ajira kwa waalimu
--
Katika
mwaka wa masomo 2009/10 jumla ya wanafunzi 19,652 walihitimu mafunzo ya
ualimu wakiwemo ngazi ya shahada 12,120 na stashahada 7,532. Kati ya
wanafunzi hao jumla ya wanafunzi 17,684 walihitimu na kufaulu masomo
yao, wenye shahada wakiwa 12,095 na wenye stashahada 5,589.
Uchambuzi wa sifa za wahitimu
17,684 waliohitimu na kufaulu mitihani yao umeonesha kuwa jumla ya
wahitimu 8,857 wametoka kazini (in-service). Idadi hiyo inajumuisha
wenye shahada 7,437 (25 kutoka Zanzibar) na wenye stashahada 1,420.
Walimu hao wamerudi kwa waajiri wao ili wapangiwe kazi kulingana na
elimu yao. Aidha, kuna wahitimu 328 kutoka Zanzibar (wakiwemo 303
tarajali na 25 kutoka kazini) ambao wanatarajiwa kuajiriwa katika shule
na vyuo vya Zanzibar. Hivyo, wahitimu wanaobakia ambao wamepangwa
kufundisha katika shule za sekondari na vyuo vya ualimu Tanzania Bara ni
8,524 wakiwemo wenye shahada 4,355 na wenye stashahada 4,169.
Kama ilivyobainishwa katika sehemu ya
kwanza ya taarifa hii, jumla ya wahitimu 8,524 waliohitimu na kufaulu
mitihani yao wataajiriwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha. Vilevile
Serikali imekubali kuajiri walimu 702 (wakiwemo 565 wenye shahada na
137 wenye stashahada) waliomaliza mafunzo yao miaka ya nyuma ambao
wameomba kuajiriwa Serikalini.
Hivyo,
jumla ya walimu wote watakaoajiriwa Serikalini kwa mwaka wa fedha
2010/2011 ni 9,226 wakiwemo wenye shahada 4,920 na wenye stashahada ni
4,306. Kati ya walimu watakaoajiriwa jumla ya walimu 9,039 wamepangwa
kufundisha katika shule za sekondari na walimu 187 wamepangwa kufundisha
katika vyuo vya ualimu.
Walimu wote wa shule za sekondari
wamepangwa katika Halmashauri mbalimbali kwa kutumia kigezo cha
upungufu wa walimu katika Halmashauri husika. Hivyo, kila mwalimu
anatakiwa kuripoti katika Halmashauri aliyopangwa kwa kuwa fedha za
mshahara wake zimekasimiwa kwenye Halmashauri alikopangwa na si
vinginevyo. Orodha ya walimu hao na Halmashauri walikopangwa zimetumwa
kwenye Mikoa na Halmashauri. Aidha, orodha hiyo inapatikana kwenye
tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi www.moe.go.tz na tovuti
ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
www.pmoralg.go.tz.
Walimu wote wapya wanaagizwa
kuhakikisha kwamba wanaripoti katika Halmashauri/ Vyuo vya Ualimu
walikopangwa ifikapo tarehe 24/01/2011. Watendaji na wasimamizi wa elimu
kwenye Halmashauri na Vyuo vya Ualimu watakuwepo kuwapokea.
Mwalimu
yeyote atakayeshindwa kuripoti kwenye Halmashauri / Chuo alikopangwa
baada ya siku saba (7) tangu tarehe anayotakiwa kuripoti atahesabika
kuwa amekataa kukubali nafasi ya ajira aliyopewa na Serikali.
Baada ya kuripoti kwenye
Halmashauri/Vyuo waajiri watatakiwa kuwajazia walimu hao Fomu maalum
zenye Taarifa ya Kiutumishi ya Mtumishi (Personal Data Form)na
kuziwasilisha Ofisi ya Rais, UTUMISHI pamoja na barua ya ajira ya
mtumishi. Taarifa hizo zikiwa katika “hard” na “soft copy” ziwasilishwe
UTUMISHI kabla au ifikapo tarehe 29/01/2011 ili watumishi hao waingizwe
katika mfumo wa malipo (Payroll). Waajiri wanakumbushwa kwamba “Computer
Data Sheet” hazitahitajika katika zoezi hili.
Waajiri(Wakurugenzi wa
Halmashauri na Katibu Mkuu–Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi)watawalipa malipo stahili kwa mujibu wa nyaraka na miongozo ya
Serikali kuhusu waajiriwa wapya.
Nawatakia utumishi mwema katika Sekta ya Elimu.
Imetolewa na:
MHE. DKT.SHUKURU J. KAWAMBWA
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
0 comments:
Post a Comment