Thursday, October 18, 2012

Wazazi walia utitiri wa michango Marian Boys

WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari ya Marian Boys iliyoko Kerege, wilayani Bagamoyo, Pwani, wamelalamikia wingi wa michango katika shule hiyo ikiwemo ya ujenzi wa madarasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii, baadhi ya wazazi wamesema uongozi wa shule hiyo unawatwisha hata majukumu ya mmiliki wa shule.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina wakihofia usalama wa watoto wao, wazazi hao walisema uvumilivu wao umefika kikomo.
Walisema hawana shida na karo na michango mingine kama chakula, sare na usafiri, bali kilio chao ni kitendo cha uongozi wa shule hiyo chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi ya shule hiyo aliyetajwa kwa jina moja la Heri kuwabebesha jukumu la mmiliki wa shule hiyo.
Walisema kila mtoto aliyekuwa akitaka kujiunga na kidato cha kwanza, alilipa sh 15,000 na wanafunzi 240 waliofaulu, walitakiwa kutoa sh 400,000 kabla ya kujiunga rasmi kwa masomo.
Walisema chini ya mpango huo, shule hiyo iliweza kutengeneza sh milioni 96 kwa ajili ya majengo, hivyo kubeba jukumu la mmiliki wa shule.
Kwa mujibu wa maelezo ya wazazi hao, uongozi wa shule uliwaeleza ni sehemu ya ada ambayo watalipa baada ya kujiunga na masomo rasmi shuleni hapo.
Wamedai kuwa baada ya watoto kuanza masomo, uongozi wa shule uliwataka kulipa ada kamili na kwamba sh 400,000 ni ada ya majengo.
Walisema jambo hilo liliwaweka kwenye wakati mgumu wazazi, lakini kwa kupenda elimu ya watoto wao, walikubali kulipa ada kamili kama ilivyotakiwa.
“Hapa tulianza kuwa na mashaka, lakini kwa kupenda elimu ya watoto wetu, tukaona basi, tuendelee, lakini hapana sasa imebidi tuseme,” alisema mmoja wa wazazi hao.
Alisema katika mazingira hayo, bado uongozi wa shule hiyo hivi karibuni uliitisha harambee ya kuchangia mabweni ya madarasa ya kidato cha tano na sita.
“Katika harambee ile, wazazi tulikuwa ni kama wahusika wakuu, kila mmoja alitakiwa kuahidi fedha, kwa mfano mimi niliahidi sh 100,000, lakini baada ya kutafakari sana, kwa kweli hadi sasa sijatoa,” alisema mzazi mwingine.
Alisema kilichowakera zaidi wazazi hadi kulalamika, ni hatua ya hivi karibuni ya uongozi wa shule hiyo kuwataka kila mzazi kuchanga sh 200,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.
Wazazi hao walisema mapema wiki hii baadhi ya wazazi wametumiwa ujumbe mfupi wa simu ukiwalisha uamuzi wa mkutano wa wazazi uliofanyika Oktoba 6, mwaka huu, kwenye ukumbi wa Msimbazi Centre, jijini Dar es Salaam.
Kupitia ujumbe huo uliotumwa kwa simu namba 0713 431264, unaeleza kilichofikiwa kwenye kikao hicho kuwa kila mzazi anatakiwa kutoa sh 200,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kwamba hadi ifikapo Desemba 31 mwaka huu wanatakiwa wawe wamekamilisha mchango huo kupitia akaunti ya shule na kwa maelezo zaidi wapige namba 0777523518.
Wazazi wamehoji mantiki ya uongozi na mmiliki wa shule hiyo waliyemtaja kwa jina moja la Father Bayo kuwachangisha wazazi hadi ujenzi wa madarasa ya shule hiyo binafsi.
Tanzania Daima ilipomtafuta mwenye namba hiyo 0777523518, alikiri yeye ni Heri, Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi wa shule ya Marian Boys.
Hata hivyo, wakati mwandishi wa habari hizo akieleza sababu ya kutafutwa kwake, simu ilikatika na kila alipotafutwa, ujumbe uliashiria alikuwa nje ya nchi.
Tanzania Daima ilipomtafuta mtumaji wa ‘meseji’ kwa wazazi, mhusika alijitambulisha kuwa ni mwalimu wa shule hiyo na alipotakiwa kutoa ufafanuzi, alisita kabla ya kumpasia simu yake aliyemtambulisha kama mkuu wa shule.
Naye mkuu wa shule, akakiri kwa ufupi uwepo wa mchango huo na kila mzazi anapaswa kulipa kupitia akaunti ya shule.
Alipoulizwa ni malipo gani hayo, alisita kidogo na kisha kusisitiza maelezo yalishatolewa.

CHANZO:TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment