Thursday, May 29, 2014

MAONESHO WIKI YA ELIMU DODOMA YAFANA


Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda (MB) amezidua wiki ya Elimu nchini iliyoanza tarehe 03 Mei hadi Mei 10, 2014 mjini Dodoma.
 
Akizindua maadhimisho hayo Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuweka msingi wa dhati katika shule za kata kwa lengo la kupandisha kiwango cha kufaulu. Amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa – Big Results Now BRN katika Sekta ya Elimu ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
 
Maadhimisho hayo yana lenga kuelimisha Umma wa Watanzania juu ya umuhimu wa Elimu Bora na ushiriki wao katika kuhakikisha kuwa elimu bora inapatikana kwa wote.
 
Maadhimisho ya Wiki ya Elimu yamejumuishwa pamoja na kuainisha, kuwatambua na kutoa Tuzo kwa Wanafunzi, Walimu, Shule, Halmashauri na Mikoa iliyofanya vizuri katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi na Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Sekondari Kidato cha 4 mwaka 2013.
 
Kwa upande wa taarifa za Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne zinaonesha kuwa, ufaulu wa juu (Daraja la I-III) kwa mwaka 2013 unaonekana kuwa mkubwa ukilinganishwa na miaka ya 2010, 2011, na 2012 kwa shule za Kata, Serikali, Binafsi na Seminari. Aidha, idadi ya watahiniwa waliofaulu katika madaraja hayo nayo iliongezeka kwa aina zote za shule.
 
Kwa upande wa Shule za Kata, Takwimu zinaonesha kuwa wastani wa ufaulu wa Shule za Kata ni mdogo (Asilimia 48 ) ikilinganishwa na Asilimia 59.7 Shule za Serikali; Asilimia 84.3Shule Binafsi na Asilimia 80.8 Shule za Seminari. Hata hivyo, kwa idadi ya wanafunzi wengi waliofaulu katika Mitihani hiyo ni wa kutoka katika Shule za Kata ambao ni 109,229 ikilinganishwa na52,242 wa Shule za Binafsi, 33,533 wa Shule za Serikali na 6,149wa Shule za Seminari. Hii inatokana na ukweli kuwa idadi kubwa ya Wanafunzi iko kwenye Shule za Kata.
 
Aidha, takwimu zinaonesha kuwa, ufaulu usioridhisha wa Daraja la Sifuri wa Shule za Kata kwa mwaka 2013 ni wa chini kuliko miaka mitatu iliyopita.
 
Kutokana na yaliyojitokeza kwenye matokeo hayo ya Kidato cha Nne mwaka 2013, ni dhahiri kwamba, Serikali inahitaji kuongeza uwekezaji kwenye shule zake za Kata na zile za Serikali kwa kasi zaidi pia kuna umuhimu mkubwa wa kuangalia upya uwekezaji kwenye shule za vipaji maalum ili kufikia malengo yayowekwa wakati wa kuanzishwa kwa shule hizo. Uwekezaji huo ulenge zaidi kwenye miundombinu, walimu, ukaguzi, vitabu, na vitendea kazi.

PICHA: Baadhi ya wanafunzi wakiwa wamekaa jukwaani wakati mgeni rasmi Waziri Mkuu Mhe.Mizengo Kayanza Peter Pinda (MB) akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa wiki ya Elimu nchini inayofanyika kitaifa mjini Dodoma kauli mbiu ya mwaka huu inasema “ELIMU BORA KWA WOTE INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO”

Waziri Mkuu amesema kwa upande wa mafanikio katika Sekta ya Elimu mwaka 2009 – 2013 Serikali imelenga kuwa na darasa la Elimu ya Awali katika kila Shule ya msingi,kuongezeka kwa idadi ya walimu,kuongezeka kwa uwiano wa mwalimu na mwanafunzi,na kuongezeka kwa shule za msingi na sekondari nchini.
 
Kuanzishwa kwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kumeleta ushindani kwa kupanga shule katika makundi ya ubora wa ufaulu na kutoa Tuzo kwa shule 3,000 zilizofanya vizuri na zilizoonesha kupiga hatua katika mtihani wa mwaka 2013. Lakini pia, Mpango huu umeweza kuinua kiwango cha ufaulu kutoka Asilimia 30.72 mwaka 2012 hadi 50.61 mwaka 2013 kwa elimu ya msingi na Asilimia 43.08 mwaka 2012 hadi Asilimia 58.25 mwaka 2013 kwa Elimu ya Sekondari.
 
Mpango wa Matokeo Makubwa sasa pia, umeimarisha usimamizi wa menejimenti ya shule kwa kuandaa kitabu cha kiongozi na kutoa mafunzo kwa Wakuu wa Shule za Sekondari 3,000. Aidha, chini ya mpango huu, wakuu wa shule wameweza kujenga uwezo wa ufundishaji na ujifunzaji kwa kutoa mitihani ya majaribio kwa Darasa VI na VII katika Elimu ya Msingi na Kidato cha IV kwenye Elimu ya Sekondari, na kusimamia uimarishaji wa miundo mbinu ya Shule 264 .
 
Waziri Mkuu ameitaka TAMISEMI kusimamia vema Fedha za ukarabati wa majengo na Wakurugenzi watakaozembea wawajibishwe.
 
Awali akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu kwa niaba ya Waziri wa Nchi OWM - TAMISEMI Naibu Waziri Nchi TAMISEMI (ELIMU) Mhe. Kassim Majaliwa amesema moja ya vipaumbele vya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa vilivyoibuliwa kwenye Maabara ya Elimu Aprili, 2013, ni utoaji wa Tuzo kwa Shule kuanzia Matokeo ya Mitihani ya Kumaliza Elimu ya Msingi na ya Sekondari ya mwaka 2013 ambapo kutakuwa na makundi mawili ya kupewa tuzo.
 
Kundi la kwanza ni shule zilizofanya vizuri na kundi la pili ni shule zilizoongeza kiwango cha ufaulu ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2012. Jumla ya shule 4,000 zitahusika katika mpango huu wa kupewa tuzo, kati ya shule hizo shule 3,000 ni za Msingi na 1,000 ni za Sekondari.
 
Amesema katika kufanikisha Maadhimisho ya Wiki ya Elimu nchini wadau mbalimbali wamejitolea na wamehaidi kujitolea kwa hali na mali. Mpaka sasa wadau hao ni pamoja na DfID, USAID, TAMONGOSCO, EQUIP-TZ, TWAWEZA na White Dent Chemi Cotex.
 
Maadhimisho ya wiki hii ya Elimu mwaka huu yenye kauli mbiu: ‘ELIMU BORA KWA WOTE INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO', yanaambatana na maonesho na shughuli mbalimbali za elimu kutoka kwa wadau wa elimu kwa muda wa wiki moja yanayoendelea katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma



PICHA: Waziri Mkuu Mhe.Mizengo Pinda akipata maelezo katika banda la Chama cha Walimu Tanzania kushoto kwake ni Mhe.Kassim Majaliwa Naibu Waziri TAMISEMI (ELIMU) wa kulia kwake ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe.Dk Shukuru Kawambwa.






0 comments:

Post a Comment