Tuesday, October 16, 2012

Mkuu wa Mkoa ahimiza masomo ya sayansi



MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, amewataka vijana waanze kusoma masomo ya sayansi, ili madaktari wengi waweze kupatikana. Sadick alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam, katika hafla ya Siku ya Afya ya Macho, iliyokuwa imeandaliwa na Benki ya Standard Chartered kwa kupitia mradi wake wa ‘kuona ni kuamini’.

Alisema kuwa, tatizo la upofu kwa binadamu linaweza kuepukika katika jamii yoyote ile bila hata kutumia gharama kwa kuzingatia usafi wa mazingira, lishe bora na kula matunda.

“Mkizingatia ushauri wa daktari na kufuata kanuni zote za afya, nadhani hakuna mtu atakayepata tatizo la macho hapa nchini, kwani haihitaji gharama yoyote.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuwapatia elimu ya upofu wananchi wote, ili walielewe kwani wakielewa hili, tatizo litapungua na kuisha kabisa japokuwa kuna wataalam wachache.

“Katika takwimu zizilizopo, zinaonyesha kuwa, kila mwaka zaidi ya Watanzania 75,000 wanapata upofu kutokana na sababu mbalimbali, hivyo Serikali ni jukumu lake kuongeza bajeti, ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Tanzania Limited, Sabi Theobald, alisema kuwa, mbali na kuendesha shughuli za biashara, pia wamekuwa mstari wa mbele katika shughuli za kuleta maendeleo katika jamii.

“Zaidi ya watu 177,000 wameweza kunufaika na mradi huo ambao hadi sasa tumetumia Dola za Marekani milioni 87.

“Sisi tumekuwa tukiangalia maeneo makuu manne kama vile elimu, afya, vijana na mazingira na pia tumekuwa na miradi mikubwa ya kukabiliana na janga la Ukimwi chini ya mradi wa Living With HIV, Ugonjwa wa Malaria chini ya Nets for life na mengineyo,” alisema Theobald.

Pia alisema kuwa, ili kuendeleza mafanikio ya benki hiyo, wamejipanga kukusanya Dola za Marekani milioni 100 ifikapo mwaka 2020, kwa ajili ya mradi wa kuona ni kuamini.

CHANZO:GAZETI MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment