Tuesday, October 30, 2012

Mkuu wa shule ampiga mwalimu mlemavu

MKUU wa Shule ya Msingi Igaka iliyopo Kata ya Buzilasoga wilayani Sengerema, Mwanza, Boniphace Shilunga, anadaiwa kumvamia ofisini kisha kumpiga ngumi mwalimu mwenzake kwa kosa la uwajibikaji kazini.
Taarifa zinadai kuwa mwalimu aliyekumbwa na zahama hiyo mbele ya walimu wenzake ni Elias Lubasha, ambaye ni mlemavu wa mguu.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao ni walimu wenzake, tukio hilo la kusikitisha lilitokea Oktoba 19 majira ya mchana.
Walisema chanzo cha tukio hilo ni mkuu huyo kuingia kwenye ofisi ambayo hutumiwa na walimu hao na kukuta wakijadili kitendo cha mkuu wao huyo kuchukua baadhi ya samani za shule na kuzipeleka kwake.
Walifafanua kuwa kitendo cha mkuu wao huyo kuingia ofisini kwa walimu na kukuta hoja hiyo, huku mzungumzaji mkubwa akiwa Mwalimu Lubasha, kilionekana kumkera, kisha mkuu huyo akamfuata mwalimu mwenzake alipokuwa amekaa na kumrushia ngumi.
“Siku hiyo sisi tulikuwa tunajadili uhalali wa mkuu wetu kutumia baadhi ya samani za shule na kuzigeuza zake kinyume cha utaratibu, ndipo alipoingia na kukuta mjadala huo wakati huo Lubasha ndiye alikuwa anachangia hoja na ndipo tuliposhangaa kuona akimrukia na kumpiga ngumi,” alisema mmoja wa walimu.
Baadhi ya samani hizo ni pamoja na viti na meza, ambapo wanadai badala ya kuwa shuleni vimekuwa vikitumiwa na mkuu huyo nyumbani kwake kinyume cha utaratibu.
Kufuatia sakata hilo, iliwalazimu walimu hao kuingilia kati na kuamua ugomvi huo kisha kuitishwa kikao cha dharura kujadili mgogoro huo, ikiwa ni pamoja na mkuu huyo kumtaka radhi mwalimu mwenzake kwa kisingizio cha ghadhabu kumpanda na kusababisha hali hiyo.
Alipohojiwa na gazeti hili shuleni hapo, Lubasha alikiri kupigwa ngumi na mkuu wake wa kazi na kudai kuwa hakuchukua uamuzi wa kumfikisha mbele ya sheria baada ya kumuomba radhi.
“Ni kweli kama ulivyoelezwa lakini baada ya tukio hilo tulikaa kikao cha ‘staff’ wote akiwemo na yeye na aliomba nimsamehe, kwa madai hasira ndiyo ilimfanya anipige, nami nimemsamehe na ndiyo maana sikulifikisha suala hilo polisi japo ni kweli alinidhalilisha,” alisema Lubasha.
Naye mkuu huyo, Shilunga alipofuatwa kujibu tuhuma hizo, aligoma kuzungumza chochote na kumtaka mwandishi kuonana na Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Paulo Yatobanga.
Yatobanga aliitaka serikali kumpa uhamisho mkuu huyo kabla madhara makubwa hayajajitokeza, kwa madai kuwa amekuwa tatizo na hana mahusiano mazuri na wenzake, kwa kuwa amekuwa akitumia rasilimali za shule pasipo kuzishirikisha kamati husika.
Alizitaja baadhi ya mali za shule ambazo mkuu huyo ameuza pasipo kushirikisha kamati husika kuwa ni pamoja na miti mitatu aina ya michongoma, mikaribea na mzambarau.
Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo, Juma Mwanjimbe, alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo, alikiri kulifahamu ila akadai kuwa walimu hao walitaka kupigana wakawahiwa kuamuliwa.
Hata hivyo alimtetea mkuu huyo, akidai kuwa amekuwa mwiba kwa walimu hao kutokana na utendaji kazi wake mzuri na ndiyo sababu za kumfanya achukiwe pale inapotokea kuwabana kazini.

CHANZO: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment